Chid Benz alifufua safari yangu kimuziki-Ditto

Msanii wa muziki wa Bongofleva ambaye kwa sasa anajishugulisha na kilimo cha mazao mbalimbali Lameck Ditto amefunguka na kusema kuwa msanii Chid Benz ndiye aliyefufua safari yake ya muziki baada ya kimya kirefu

 
 Akiongea na East Africa Radio Ditto amesema kuwa alipigiwa simu na Chid Benz aende studio ya Dhabu Records na alipokwenda alikutana na mdundo wa wimbo wa 'Dar es Salaam Stand Up' ndipo alipopata mzuka wa kufanya Chorus kali ya wimbo huo ambao ulipokelewa vizuri sana na mashabiki na kuwa wimbo mkubwa.
"Nilikuwa nipo kimya muda mrefu sana, ghafla nikaona simu ya Chid akaniita studio na nilipofika nilipewa mdundo uliokuwa mkali sana jambo ambalo lilinifanya nipatwe na mizuka ya kufanya kazi ile kwa muda mfupi, na kupitia wimbo ule ndipo safari yangu ya kwenye muziki ilifufuka tena," alisema Lameck Ditto.
Ameongeza kuwa anakumbuka kabisa wimbo wa 'Dar es Salaam Stand Up' ulikuwa wimbo wake wa pili kufanya na msanii mkubwa nchini. Msanii Ditto kwa sasa ameegemea zaidi katika masuala ya kilimo japo hata sanaa anafanya lakini kwa sasa nguvu yake kubwa ameielekeza katika kilimo.

No comments:

Post a Comment