Luvuki amtwisha Nyalandu mgogoro wa Mbonipa.



Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
 Serikali imewaagiza wakazi wa vijiji  21 vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Mali Hai Tarafa ya Idodi na Pawaga (Mbonipa), viongozi wao na mmoja wa wawekezaji wake kukutana kujadili na kutatua mgogoro unaofukuta baina yao ili kupata mwafaka.

 
Agizo hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (pichani), kwenye kikao cha wenyeviti wa vijiji hivyo na wadau wa maliasili na utalii kilichofanyika kwa lengo la kujadili mgogoro huo. 
 
 Nyalandu aliwataka Wanambomipa kuzungumza na wawekezaji na kupitia mikataba baina yao  huku akisisitiza kuwa serikali haitakubali iendelee kutumika endapo itabainika kuwa na dosari.
 
 Nyalandu aliyeongozana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi na Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na viongozi wengine alisema:
 
“Nimejaribu kuangalia mgogoro huu nimeona hisia zenu na nimegundua na inabidi serikali ihakikishe kila mtu anapata haki yake," alisema na kuongeza kuwa:
 
"Nilichogundua kuna wananchi ambao wamekosa fedha zao kutoka kwa mwekezaji ambazo hazijalipwa muda mrefu, kuna rasilimali za kwenu ambazo hamjazifaidi na badala yake wanafaidi wengine. ”
 
Vilevile aliagiza mkataba na mwekezaji yoyote Duniani anayetaka kuwekeza vitalu vya uwindaji nchini ni lazima ipitiwe na serikali kabla ya kusainiwa na mwekezaji huyo ili kujiridhisha haiwanyonyi wananchi kwa manufaa ya wachache.
 
 “Mikataba lazima niione kupitia wanasheria wangu wizarani, tuipitishe na kama tunaona mkataba una matatizo  tutaurudisha na kuwaambia vipengele hivi vinawanyonya wananchi na hivyo vibadilisheni,” alisisitiza Nyalandu
 
Awali alisema mgogoro huo unatokana na Mbomipa kudhani kuna uonevu uliotokana na mikataba ilivyofanyika, Mbomipa kulaumu halmashauri kuu ama mfumo wa uendeshaji ambao ndiyo uliowafikisha hapo.
 
 Hata hivyo, aliwataka wanajumiya hiyo kuhakikisha kukutana na kupitia upya mifumo ya utawala ili baadaye iwe mfano wa kuigwa na jumuiya nyingine kama hiyo nchini.
 
Kwa upande mwingine, aliwashauri Mbomipa kukutaka na mwekezaji anayedaiwa kuwa chanzo cha mgogoro huo kukubalina kuiondoa kesi yao mahakamani.
 
" Hii ndiyo njia yangu yakuweza kuwasaidia ili mgogoro huu uweze kumalizika kwa sababu taarifa niliyoipata mwekezaji alikubali kukaa na Wambomipa," alisema.
 
Kwa upande wake, Waziri Lukuvi, alionyesha kushangazwa na mwekezaji huyo kukaidi zuio la mahakama kwa kuendelea kuwinda wanyama.
 
Vilevile alimhoji Waziri Nyalandu sababu za wizara yake kuendelea kutoa kibari cha uwindaji bila kutoa fedha kwa wanavijiji hao.
 
Lukuvi alisema wamemuita Waziri Nyalandu kwa lengo la kumaliza mgogoro huo na wanavijiji hao, hivyo walipwe fedha zinazolingana na kile kinachowindwa.
 
Mbomipa imeingia katika mgogoro huo baada ya kumtuhumu mwenyekiti wao, Phillip Mkubata kushindwa kuendesha jumuiya hiyo kwa kuzingatia katiba, kanuni, taratibu na kushindwa kuitisha mikutano ya kikatiba kwa miaka miwili.
 
 Tuhuma nyingine ni kubadili  matumizi ya moja ya eneo la uwekezaji la jumuiya hiyo lililotengwa kwa ujenzi wa kambi na hoteli za kitalii na kuwa la uwindaji wanyamapori bila ridhaa ya mkutano mkuu wao.
 
 Eneo hilo la kanda ya uwekezaji ya Lunda sehemu yake ya kilomita mbili za mraba, lilitolewa kwa kampuni ya uwindaji kwa ajili ya ujenzi wa kambi na hoteli za kitalii bila kutangazwa ili kuruhusu ushindani kama sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 inavyotaka.
 
  Wanajumuiya hao waliendelea kumtuhumu mwenyekiti huyo kwa kushindwa kusimamia makusanyo na kutoa gawio kwa vijiji kila mwaka  huku akishindwa kukusanya mapato ya zaidi ya Sh. milioni 200 kwa kampuni hiyo ambayo ilikabidhiwa eneo kwa zaidi ya miaka 10.
 
 Mbomipa ni eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 776.4 la hifadhi ya jamii ya wanyamapori linalopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo Wilaya ya Iringa mkoani Iringa likiwa na wanyamapori

No comments:

Post a Comment