UBAGUZI WA RANGI, MGOGORO WA KITAIFA MAREKANI

Spika wa Bunge la Baraza la wawakilishi nchini Marekani, John Boehner.
Kufuatia kuongezeka ghasia zitokanazo na ubaguzi wa rangi Marekani, Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi nchini humo amesema uhusiano baina ya Wamarekani wenye asili ya Afrika na maafisa wa polisi sasa umegeuka na kuwa mgogoro wa kitaifa.
Waandamanaji wakiharibu gari la polisi.
John Boehner katika mahojiano na Televisheni ya NBC amesisitiza kuwa maafisa wa usalama wa umma hawapaswi kujihusisha na vitendo vya utumiaji mabavu. Marekani hivi sasa imekumbwa na mgogoro wa kitaifa. Hiyo ni kauli ya kiongozi nambari tatu Marekani baada ya rais na makamu wake.
Katika mgogoro huo, mamilioni ya Wamarekani weusi au wenye asili ya Afrika daima wananyanyaswa na kufanyiwa ukatili wa maafisa wa usalama na polisi wazungu. Katika kipindi cha mwaka moja uliopita, kumeshuhudia visa kadhaa vya polisi wazungu wakiwafyatulia risasi na kuwaua kiholela Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Katika vitendo hivyo vya unyama na ukatili, polisi huwalenga na kuwafyatulia risasi washukiwa ambao aghalabu huwa vijana na mabarobaro. Katika kitendo cha hivi karibuni cha ukatili huo wa polisi Freddie Gray, Mmarekani mweusi baada ya kutiwa nguvuni na polisi mzungu alipigwa na kuadhibiwa vikali ndani ya gari la polisi na kisha kukimbizwa hospitali kutokana na majeraha aliyoyapata.
Akiwa hospitalini alifariki dunia. Kufuatia tukio hilo, mji wa Baltimore umeshuhudia machafuko makali zaidi ya mitaani ambapo wananchi wenye hasira wamejitokeza kulaani ukatili wa polisi wa Marekani. Machafuko hayo yametajwa kuwa mabaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Waandamanaji wakiwa na mabango.
Ikumbukwe kuwa katika historia ya Marekani kumeshuhudiwa uasi na maandamano ya Wamarekani weusi wakilalamikia ubaguzi wa rangi nchini humo. Kilele cha malalamikio hayo kilikuwa katika miongo ya 1950 na 1960 ambapo mashinikizo yalipelekea kuidhinishwa sheria kadhaa ikiwemo sheria ya kuwapa Wamarekani weusi haki ya kupiga kura.
Pamoja na hayo, hivi  sasa baada ya kupita zaidi ya miaka 50 tokea kuibuka mapambano ya haki za kijamii Marekani, Wamarekani wenye asili ya Afrika wangali wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa na dhulma zisizo na kikomo. Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hivi sasa maafisa kadhaa wazungu katika kikosi cha polisi Marekani wamefyatuliwa risasi katika kile kinachotajwa kuwa ni ulipizaji kisasi.
Weledi wa mambo wanasema hali kama hivyo itaitumbukiza Marekani katika mgogoro mkubwa sana wa kiusalama. Marekani ni moja za nchi zenye idadi kubwa zaidi ya silaha ndogo ndogo miongoni mwa raia. Inakadiriwa kuwa katika kila Wamarekani watatu, mmoja au wawili kati yao wana silaha.
Polisi wakiimalisha ulinzi.
Idadi kubwa ya silaha hizo pia ziko mikononi mwa Wamarekani wenye asili ya Afrika na wasiokuwa wazungu. Kwa msingi huo inadokezwa kuwa iwapo maandamano hayatapelekea kumazilika vitendo vya ubaguzi wa rangi na ukatili wa maafisa wazungu katika vikosi vya usalama, basi natija itakuwa ni kuanza mapambano ya silaha mitaani.
Jamii ya Marekani hivi sasa katika upande moja inakabiliwa na matatizo makubwa ya ubaguzi wa rangi na katika upande wa pili inakumbwa na mgogoro wa kiuchumi na kupungua kiwango cha maisha bora katika jamii na hayo yote yamepelekea kuongezeka mashinikizo ya kila aina.
Ni kwa sababu hii ndio weledi wa mambo wanasema Marekani sasa iko katika dimbwa kubwa la mgogoro wa kijamii ambao unaweza kuwa hatua ya kwanza ya mapinduzi au hata vita vya kitabaka na kirangi. Hatua ya John Boehner, Spika wa Baraza la Wawakilishi ambaye ni kiongozi nambari tatu nchini Marekani kutumia ibara ya ‘mgogoro wa kitaifa’ katika kufafanua kuhusu machafuko ya ubaguzi wa rangi hivi sasa nchini humo ni kengele ya hatari kuhusu kuibuka umwagikaji damu nchini humo.

No comments:

Post a Comment