Chadema, Polisi watunishiana misuli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo.
 Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limeyapiga marufuku maandamano ya wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) yaliyopangwa kufanyika leo, huku chama hicho kikisema yako pale pale.
 
Maandamano hayo yameandaliwa kwa ajili ya kushinikiza kutolewa kwa taarifa za matumizi ya Sh. milioni 720 za mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya Msamvu.  
 
Wiki iliyopita Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Wilaya ya Morogoro, James Mkude, kilitangaza kufanya maandamano hayo hadi katika uongozi wa Manispaa ya Morogoro kushinikiza  Mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood (CCM), 
 
apewe taarifa za matumizi ya fedha za mradi wa ujenzi huo baada ya kunyimwa na uongozi wa Manispaa wakati wa ziara yake  ya kukagua mradi huo. 
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema jana kuwa taarifa aliyoitoa Mkuu wa Polisi wilaya ya Morogoro ambaye ndiye mwenye dhamana ya kutoa ulinzi kufanyika ili maandamano hayo yafanyike  imeonyesha kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani endapo maandamano hayo yataruhusiwa, hivyo yamepigwa marufuku.
 
 “Nina copy (nakala) hapa nimeletewa na OCD wangu, kuwa maandamano hayo hayaruhusiwi kutokana na uchunguzi wake aliofanya kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani endapo yatafanyika, mimi sitaki malumbano na viongozi wa kisiasa, naomba waheshimu utaratibu pamoja na sheria zilizopo,” alisema.
 
 Alisema kuwa siyo lazima kufanya maandamano kwa ajili ya kushinikiza kupewa taarifa hizo za matumizi ya fedha za ujenzi wa stendi hiyo bali ipo njia mbadala kwa viongozi hao wa Chadema ni kwenda kwa uongozi wa Manispaa ya Morogoro au ule unaohusika kuomba kupatiwa taarifa hizo ili kuwaeleza wananchi katika mikutano yao.
 
“Sisi kama Jeshi la Polisi tutahakikisha tunasimamia sheria kwa kuwa tunajua maandamano yamepigwa marufuku, ninawataka Chadema kuheshimu maamuzi yaliyotolewa kuhusu kutofanyika kwa maandamano hayo,” alisema Kamanda Paul.
 
Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwenendo wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, Dk. Albanie Marcossy, alisema kuwa maandamano hayo yapo pale pale kwa kuwa kisheria wao wanapaswa kutoa taarifa tu kwa jeshi hilo na sio kuomba kibali.
 
 Alisema kuwa wao hawaogopi polisi kuwafyatulia mabomu na kuwataka waandae mabomu ya kutosha kwakuwa wao wanatetea maslahi ya wananchi ambao wamekuwa wakikatwa kodi huku fedha hizo zikiliwa na wajanja wachache.
 
 Meneja wa mradi wa ujenzi wa kituo cha Msamvu Property Company Limited, Stanley Mhapa, alisema hakuna ubadhilifu wa aina yoyote katika mradi huo wa ujenzi wa stendi na taarifa za ukaguzi zipo wazi na kutaka yoyote mwenye mashaka aende kupata ukweli wa matumizi ya fedha hizo.

No comments:

Post a Comment