LHRC CHATOA TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MWENENDO NA HATUA ZA KISHERIA KWA VIONGOZI WA UMMA WANAOKIUKA MAADILI

 Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, wakati akitoa taarifa juu ya mwenendo na hatua za kisheria kwa viongozi wa umma wanaokiuka maadili.Katikati ni Mkurugenzi wa Ujengaji Uwezo na Uwajibikaji wa LHRC, Imelda Urrio na kulia ni Ofisa Programu Dawati la Waangalizi Watendaji wa Serikali wa LHRC, Hussein Sengu.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 
 
Na Dotto Mwaibale
 
SERIKALI imepoteza sh.bilioni 250 kwa kipindi cha miaka 9 kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma, ikiwemo rushwa na ubadhilifu wa mali mbalimbali.
 
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba Dar es Salaam leo asubuhi wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya mwenendo na hatua za kisheria kwa viongozi wa umma wanaokiuka maadili.
 
“Katika kisichozidi miaka 9 kumeripotiwa kashfa kubwa nne ambazo kwa ujumla wake zimeisababishia taifa hasara ya zaidi ya sh. bilioni 250 ambapo kwa wastani inapoteza takribani asilimia 20 ya bajeti yake ya mwaka” alisema Sungusia.
 
Sungusia alizitaja kashfa hizo kuwa ni pamoja na mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada iliyotumika kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza, wizi wa mabilioni katika akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), mkataba usio na tija kwa taifa na kampuni ya Richmond, kashfa ya mabilioni ya pesa waliogaiwa viongozi wa juu kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Alisema licha ya kuwepo vyombo vya kusimamia maadili ya viongozi wa umma haliminaendelea kuwa mbaya siku hadi siku kwani rushwa inaendelea kushamiri na matumizi mabaya ya rasirimali za umma na viongozi wameendelea kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
 
Sungusia aliongeza kuwa bado kauli za kejeli na dharau zimeendelea kutolewa na viongozi wanatuhumiwa na zaidi ya yote hata mapendekezo yaliyowekwa katika rasimu ya pili ya katiba na Tume ya Kukusanya maoni juu ya maadili ya viongozi yametolewa.
 
Alisema pamoja na kuwepo na Katiba na Sheria yenye muongozo juu ya maadili ndani ya muongo huu kumekuwepo na matukio makubwa ya ukiukwaji wa maadili kwa viongozi wa umma ambapo viongozi wetu wamekuwa na matumizi mabaya ta rasilimali za umma pamoja na kujilimbikizia fedha na mali kinyume cha sheria.
 
Aliongeza kuwa pamoja na angalizo la kikatiba jitihada za Bunge kama muhimili wenye dhamana ya kusimamia serikali zimekuwa zikikwamishwa na Serikali.
 
“Mwenendo wa kuweka pingamizi Mahakama kuu kuzuia baraza la maadili kufanya kazi yake kikatiba limeonesha mwanya na udhaifu wa sheria na vyombo vya kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
 
Alisema kwa kuwa  sekretarieti inaundwa kikatiba inakazi, nguvu na mipaka yake na inatakiwa kutoingiliwa pale inapokuwa inashughulikia masuala ya kimaadili.
 
Aliongeza kuwa kwa mapingamizi yaliyotolewa na kusababisha baraza lisiendee na kazi yake kama ilivyopangwa inaonesha wazi ni jinsi gani vyombo vya kusimamia maadili ya viongozi vinavyopuuzwa.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)

No comments:

Post a Comment