Wanajeshi wa UN wasombwa na maji-Darfur

Wanajeshi wa kutunza amani wa UN nchini Sudan.
Wanajeshi wanne wa kutunza amani wa Umoja katika eneo la Darfur nchini Sudan hawajulikani waliko baada ya kusombwa na mafuriko.

Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, Rania AbdulRahman, amesema kuwa wanajshi hao walikuwa wakisindikiza msafara wa magari ya kutoa misaada, wakati waliposombwa na maji.
Afisa huyo amesema kuwa wanajeshi wengine wawili walipatikana wakiwa hai na kundi la uokoaji
Shirika la Umoja wa Mataifa wa Afya Duniani WHO, limesema kuwa zaidi ya watu laki tatu nchini Sudan, wameathiriwa na mafuriko na zaidi ya watu hamsini wamefariki mwezi huu.
Shirika hilo limesema kuwa eneo linalokaribia mji mkuu wa Khartoum ndilo limeathirika zaidi na mafuriko hayo ambayo ndiyo mabaya zaidi kuwahi kukumba eneo hilo kwa zaidi ya miaka ishirini na mitano iliyopita.

Wanajeshi wakwama kwenye mto

Kikosi cha Umoja wa Mataifa na kile cha Muungano wa Afrika katika eneo hilo la Darfur, UNAMID, ndilo kubwa zaidi duniani na lina zaidi ya wanajeshi elfu ishirini.
Mafuriko nchini Sudan
Wanajeshi hao wa kutunza amani walikuwa wakielekea eneo la Misterei, takriban kilomita hamsini, Kusini Magharibi mwa mji mkuu wa eneo hilo Geneina, na msafara wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, wakati msafara wao uliposomba na mafuriko.
Msemaji wa WFP Amor Almagro amethibitisha kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la WFP waliokuwa kwenye msafara huo, watano kati yao raia wa Sudan na wawili wa mataifa ya Kigeni wako salama.
Umoja wa Mataifa haujatoa majina au uraia wa wanajeshi hao ambao hawajulikani waliko.
Mwaka uliopita, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, alilieleza baraza la usalama la Umoja huo kuwa wanajeshi watatu kutoka Tanzania walizama majini baada ya gari lao la kijeshi, kukwama katika mto mmoja nchini Sudan.
Katibu huyo mkuu vile vile alilieleza baraza hilo kuwa kikosi chake nchini Sudan kinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kutosha na vya kisasa, hali ambayo inaadhiriwa juhudi zao za kutunza amani katika eneo hilo la Darfur.
Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa, wako katika eneo hilo la Darfur, kujaribu kumaliza mzozo uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu laki tatu wameuawa kwenye mzozo huo wa Darfur.

No comments:

Post a Comment