Syria yakana kutumia silaha za kemikali



Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria wakiwa katika hospitali moja mjini Damascus
Waziri wa mambo ya nje wa Syria , Walid Maullem, amesema anapinga vikali madai kuwa wanajeshi wa serikali ya Syria walitumia silaha za kemikali.

Maullem, aliyasema hayo mjini Damascus, baada ya Marekani kudai kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa silaha za kemikali zilitumika nchini humo.
Bwana Maullem, amesema wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, wameshindwa kufika katika eneo la pili linalodaiwa kushambuliwa kwa silaha hizo, baada ya kuzuiliwa na wapiganaji wa waasi.
Marekani na washirika wake wanajadili uwezekano wa kuanzisha mashambulio dhidi ya Syria kufuatia madai ya shambulio hilo la kemikali lililotokea wiki iliyopita.
Waziri huyo amewaambia waandishi wa habari, kuwa ikiwa nchi yake itashambuliwa kijeshi, kwa misingi ya kuwepo kwa silaha za kemikali, itakuwa kwa visingizio vya uongo na jambo ambalo halina msingo wowote.
Amekariri kuwa serikali ya Syria imetimiza ahadi zote ilizotoa kwa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuruhusu wachunguzi wake kufika nchini humo na pia kuwapa ulinzi
Awali serikali za Urussi na Uchina, kwa mara nyingine tena zimetoa onyo dhidi ya kutumia nguvu za kijeshi kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa la Syria.
Onyo hilo limetolewa huku Marekani na washirika wake wakijadili uwezekano wa kuanzisha mashambulio dhidi ya Syria, kujibu shambulio lililotokea wiki iliyopita.

Wachunguzi wa UN washambuliwa

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urussi amesema, jaribio lolote la kutoshirikisha baraza la usalama la Marekani na kubuni kila alichokitaja kama visingizio ambavyo havina msingi, litakuwa na athari kubwa katika mzozo huo.
Utawala wa Moscow vile vile umeshutumu uamuzi wa Marekani wa kuhairisha mazungumzo ya kujaribu kutatua mzozo huo wa Syria.
Msafara wa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria
Wachunguzi hao wa Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kuendelea na uchunguzi wao hii leo kwa siku ya pili mfululizo, viungani mwa mji mkuu wa Damascus.
Jopo hilo la Umoja wa Mataifa lilishambuliwa kwa risasi hiyo jana na mtu mmoja ambaye aliwavizia Magharibu mwa Damascus.
Shirika la habari la Serikali ya Uchina, Xinhua, limesema kuwa mataifa ya Magharibi, yamechukua uamuzi wa haraka kuhusu nani aliyehusika na utumizi wa silaha za kemikali nchini Syria hata kabla ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kukamilisha uchunguzi wao.
Hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, alitoa matamshi makali kuhusu madai kuwa silaha za kemikali zimetumika nchini Syria na kusema kuwa waliohusika ni sharti wawajibishwe.

No comments:

Post a Comment