HONGERA YANGA KWA KUTWAA NGAO YA JAMII KWA KUWAPIGA AZAM FC RISASI 1-0… LAKINI JICHO LA TATU LIMEBAINI UBORA WA LUHENDE NA UGONJWA WA TAIFA WA UBUTU WA SAFU YA USHAMBULIAJI !!


Wakati mashabiki wakifurika kwa wingi kwenda kuutazama mchezo wa ngao ya jamii hapo jana baina ya mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara, klabu ya Yanga dhidi ya Makamu bingwa, Wana Lambalamba Azam fc katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, binafsi sikwenda kushangilia timu yoyote bali nilienda kushuhudia mambo makubwa mawili.
Mechi ya jana kwa upande wangu ilikuwa burudani kubwa sana kwani nilishuhudia soka safi la ushindani, kwani timu zote “zimefundwa” kiukweli.
Maarifa ya makocha wawili wa kizungu, Ernie Brandts kwa Yanga na Sterwart John Hall wa Azam, yanaonekana kuwakolea vijana wa Kitanzania na nje ya Tanzania wanaozichezea timu hizo mbili.
Ukihusianisha majina ya “Yanga na Azam fc” hayana ushindani, na hii inatokana na Yanga kuwa klabu kongwe zaidi hapa Tanzania na imejiimarisha kwa kuwa na mashabiki lukuki zaidi ya Azam ambao ndio kwanza wameanza safari yao, lakini kwa kuangalia aina ya mpira unaochezwa na timu hii yenye makazi yake Chamazi, najiridhisha kuwa ni timu bora iliyojipanga na itafika mbali.
Inafahamika kuwa mechi ya jana hiyo ilimazika kwa Yanga kushinda kwa bao 1-0, bao likifungwa na Salum Abdul Telela katika dakika ya pili tu, watoto wa mjini huita “Dakika za Asubuhi”, kwangu mimi matokea hayana maana sana, lakini  nilijivuta kwenda uwanja wa Taifa kwa  mambo mawili kama nilivyosema hapo juu.
Ngao

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub “Canavaro” akipokea ngao ya jamii kutoka kwa mgeni Rasmi, mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Said Meck Sadick
Kwanza, nilienda kumuangalia bwana mdogo aliyeshutumiwa na mashabiki wengi wa soka nchini kwa kusababisha penati na kuwa uchochoro wakati  Taifa Stars ilipofungwa na Uganda mabao 3-1 jijini Kampala kuwania kucheza fainali za CHAN,  huyu si mwingine bali ni kinda David Luhende.
Watu walizungumza sana juu ya uwezo wake,wengine walisema kocha Kim alikosea kumpanga mechi yake ya kwanza Taifa Stars  dhidi ya Uganda, mechi kubwa ya mashindano na alikuwa uchochoro, lakini wakasahau kuwa hata “Mbuyu ulianza kama mchicha”. Binafsi nilijiridhisha kuwa atakuwa bora zaidi kwa uwezo alioonesha kwa siku ya kwanza, licha ya kuwa na mapungufu.
LUHENDE & MSUVA
DAVID LUHENDE
Naupenda sana msemo wa kocha wa klabu ya Mbeya City ya jijini Mbeya, Juma Mwambusi, huwa anasema “Mchezaji yeyote mwenye uzoefu alianza kutokuwa na uzoefu, akapewa nafasi akacheza na baadaye kupata uzoefu, hivyo lazima wachezaji wote wapate nafasi ya kucheza ndipo wajenge uzoefu, usipompa nafasi kijana atatoa wapi uzoefu”?.
Nina uhakika hata kocha wa Stars, Kim Poulsen ana falsafa hiyo ya kuwaamini wachezaji vijana na kuwapa majukumu mazito kama alivyofanya kwa David Luhende ambaye aliitwa kwa mara ya kwanza Taifa stars mwezi uliopita na kucheza mechi ngumu ya mashindano dhidi ya Uganda.
Ukitaja jina la Luhende, wapenda michezo wengi waliokuwa na malengo ya kwenda Afrika kusini kushuhudia fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi za ndani, CHAN nywele zinawasisimka kutokana na madudu aliyofanya nyota huyo kinda baada ya kuitwa kuziba pengo la Shomary Kapombe aliyekwenda Ulaya kujaribu bahati yake ya kucheza soka la Mataifa.
Luhende alikuwa uchochoro vibaya sana kwani alipitisha mipira mingi ya hatari na kuunawa mpira katika eneo la hatari na mwamuzi kuwazawadia mkwaju wa penati Uganda na kufunga bao la pili kupitia kwa nyota wao Brian Majwega na kuwachanganya stars waliolala kwa mabao 3-1.
Jana bila kuwa na roho ya kinyongo,  bila kujali unazi wa timu, Luhende alipiga mpira mkubwa sana na ilikuwa burudani kubwa wanapokutana na Khamis Mcha “Vialli” wa Azam, ufundi mkubwa ulioneshwa na hii inaashiria hatari kwa beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Samwel Joshua.

No comments:

Post a Comment