NI
NANI hupata kazi bora? Je, ni yule anayestahili zaidi? “La hasha,”
anasema Brian, mshauri wa kazi. “Mara nyingi yule anayetafuta kazi
akitumia mbinu nzuri ndiye hufanikiwa.” Unaweza kutumia mbinu gani
kutafuta kazi? Haya hapa ni madokezo matano.
1. Uwe Mwenye Utaratibu
Ni
rahisi kuvunjika moyo ikiwa umepoteza kazi nzuri au hujaajiriwa kwa
muda fulani. Katharina, mfanyabiashara ya soko la mtandao aliyeko hapa
Dar es Salaam anasema, “Nilipopoteza kazi, nilitumaini kwamba nitapata
nyingine. Lakini nilishuka moyo kadiri miezi ilivyopita bila kupata
kazi. Mwishowe, hata ilikuwa vigumu kwangu kuzungumza kuhusu jambo hilo
na rafiki zangu.” Hakika alikuwa alikuwa amekata tamaa.
Aliwezaje
kukabiliana na hisia za kukata tamaa? Kitabu Get a Job in 30 Days or
Less kinasema, “Inafaa upange ratiba yako kama ‘siku ya kazi’ ya kawaida
ili uanze siku ukijua unapaswa kufanya nini.” Waandishi wa kitabu hicho
wanapendekeza kwamba “uweke miradi ya kila siku na uandike
ulichotimiza.” Kwa kuongezea, wanasema kwamba “kila siku unapaswa kuanza
kwa kuvalia kana kwamba unaenda kazini.” Kwa nini? “Kuvalia inavyofaa
kutafanya uweze kujiamini zaidi hata unapozungumza kwenye simu.”
Unapaswa
kuona kazi ya kutafuta kazi kuwa ndiyo kazi yako, haidhuru itakuchukua
muda mrefu kadiri gani. Katharina, aliyetajwa hapo awali alifuata
utaratibu huo. Anasema hivi: “Nilipata anwani na namba za simu za
waajiri kutoka kwenye ofisi ya serikali ya kusaidia watu kupata kazi.
Nilijibu matangazo yaliyochapishwa kwenye magazeti. Nilichunguza kitabu
cha simu na kuandika orodha ya kampuni ambazo zingeweza kuwa na nafasi
za kazi ambazo bado hazikuwa zimetangazwa, kisha nikawasiliana nazo. Pia
niliandika habari fupi kuhusu elimu na ujuzi wangu na kuituma kwa
kampuni hizo.” Baada ya kutafuta kazi akitumia utaratibu huo, Katharina
alipata kazi nzuri.
2. Tafuta Kazi Ambazo Hazijatangazwa
Mvuvi
mwenye wavu mkubwa zaidi ndiye mwenye uwezekano mkubwa wa kuvua samaki.
Vivyo hivyo, kujua jinsi ya kupanua “wavu” wako kutafanya uwe na
uwezekano mkubwa wa kupata kazi. Ikiwa unatafuta kazi kwa kujibu tu
matangazo yaliyo kwenye magazeti au kwenye Intaneti, huenda ikawa
unapitwa na kazi nyingi. Ukweli ni kwamba kazi nyingi hazitangazwi.
Unawezaje kutafuta kazi hizo?
Mbali
na kujibu matangazo kama alivyofanya Katharina, unapaswa kutenga wakati
kila juma wa kupiga simu kwa kampuni ambazo unafikiri huenda zikawa na
kazi unazoweza kufanya. Usingoje hadi kazi hizo zitangazwe. Meneja
akikuambia kwamba hakuna kazi, mwulize ikiwa anajua kampuni zilizo na
nafasi za kazi na mtu unayepaswa kuzungumza naye. Akipendekeza kampuni
fulani, panga kuwasiliana na kampuni hiyo ukitaja jina la mtu
aliyekutuma.
Wapo baadhi ya
marafiki zangu waliopata kazi kwa njia hiyo. Mmoja wa marafiki hao kwa
jina la Tony alinieleza hivi: “Niliwasiliana na kampuni hata ingawa
hazikuwa zimetangaza nafasi za kazi. Kampuni moja ilisema kwamba haikuwa
na nafasi zozote wakati huo lakini ikaniambia nijaribu tena baada ya
miezi mitatu. Nilifanya hivyo na nikapata kazi.”
Rafiki
yangu mwinine aitwaye Anna anayeishi Mwanza, alitumia mbinu kama hiyo.
Anasema: “Nilipokuwa nikihudhuria masomo ya kutoa huduma ya kwanza,
niliona jengo jipya likijengwa upande ule mwingine wa barabara na
nikagundua kwamba litakuwa pango la ofisi. Nilijaribu mara kadhaa
kukutana na msimamizi wa msimamizi wa jengo hilo. Mwishowe aliniambia
kwamba hakukuwa na nafasi za kazi wakati huo. Hata hivyo, nilirudi mara
kwa mara ili kuona kama ninaweza kufanya kazi mahali hapo, hata kama ni
ya kujitolea. Hatimaye, niliajiriwa kazi ya muda. Nilifanya kazi zozote
nilizopewa kwa bidii. Kwa sababu hiyo, nilipata ujuzi zaidi na kupata
kazi ya kudumu kwenye moja ya makampuni yaliyokuwa na ofisi zao mule.”
Pia
unaweza kuwauliza marafiki wako, familia, na watu wengine wakusaidie
kutafuta kazi ambazo hazijatangazwa. Hivyo ndivyo Jacob, ofisa wa fedha
katika shirika moja huko Arusha alivyopata kazi. Anasema: “Wakati
kampuni niliyokuwa nikifanyia kazi ilipofilisika, niliwajulisha marafiki
na watu wa familia kwamba ninatafuta kazi. Siku moja rafiki yangu mmoja
alisikia mazungumzo fulani alipokuwa katika foleni ya kulipia bidhaa
zake kwenye super market. Mwanamke mmoja alikuwa akimwuliza mwenzake
ikiwa anajua mtu yeyote anayetafuta kazi. Rafiki yangu aliingilia
mazungumzo hayo na kumwambia kunihusu. Mipango ilifanywa na nikapata
kazi hiyo.”
3. Uwe Mwenye Kubadilika
Ili
uongeze nafasi za kupata kazi, lazima uwe mwenye kubadilika.Edwin,
ambaye ni Afisa utumishi katika moja ya benki kubwa hapa nchini yeye
husisitiza: “Kuna uwezekano mkubwa kwamba hutapata kazi unayotarajia.
Unapaswa kujifunza kuridhika na kazi isiyopatana na matarajio yako.”
Kuwa
mwenye kubadilika kunamaanisha kutochagua kazi fulani. Mfikirie Ericka,
anayeishi Dar es Salaam. Ingawa alisomea kazi ya katibu muhtasi,
mwanzoni hakuweza kupata kazi aliyotaka. Anasema: “Nilijifunza kukubali
kazi yoyote inayofaa. Kwa kipindi fulani nilifanya kazi ya kuuza vitu
dukani. Pia niliuza chapati barabarani na kusafisha nyumba. Mwishowe,
nilipata kazi ambayo nilikuwa nimesomea.”
Mary,
mmoja wa rafiki zangu wa karibu sana, aliwahi kuachana na kazi yake ya
ukarani, aliona umuhimu wa kubadilikana. Anaeleza: “Sikusisitiza kwamba
lazima nipate kazi ileile ambayo nilikuwa nikifanya. Nilichunguza kila
kazi niliyotajiwa, hata kama ilikuwa kazi ambayo watu huiona kuwa ya
hali ya chini. Kwa sababu hiyo, nilifaulu kupata kazi iliyoniwezesha
kuwategemeza watoto wangu wawili.”
4. Toa Habari Kamili Kuhusu Elimu na Ujuzi (CV)
Wale
wanaotoa maombi ya kazi za usimamizi, lazima waandike na kusambaza
habari kuhusu elimu na ujuzi wao. Lakini hata iwe unatafuta kazi gani,
habari kamili kuhusu elimu na ujuzi ulio nao inaweza kusaidia sana.
Nigel, mshauri wa kazi kwa muda mrefu, anasema: “Habari kuhusu elimu na
ujuzi wako huwafahamisha waajiri juu yako na mambo ambayo umetimiza na
kwa nini wanakuhitaji.”
Utaandika
habari gani? Andika jina lako kamili, anwani, namba ya simu, na anwani
ya barua-pepe. Taja lengo lako. Taja elimu uliyo nayo na pia mazoezi na
stadi ambazo umepata zinazohusiana na kazi unayotafuta. Toa habari
kamili kuhusu kazi ambazo umefanya hapo awali. Taja ulichofanya na pia
miradi uliyofikia na manufaa uliyoletea kampuni uliyokuwa ukifanyia
kazi. Pia taja mambo uliyofanya katika kazi yako ya awali ambayo
yanafanya ustahili kazi unayotafuta. Tia ndani habari za kibinafsi
zinazofafanua sifa na mapendezi yako. Kwa kuwa mahitaji ya kampuni
hutofautiana, huenda ukahitaji kubadili habari unazotoa kila unapotoa
maombi ya kazi.
Je, unapaswa
kutoa habari kuhusu elimu na ujuzi wako ikiwa unatafuta kazi kwa mara
ya kwanza? Ndiyo! Huenda umefanya mambo mengi yanayoweza kuonwa kuwa
ujuzi wa kazi. Kwa mfano, je, unapenda useremala au labda kurekebisha
magari makuukuu? Unaweza kutaja mambo hayo. Je, umewahi kufanya kazi
yoyote ya kujitolea? Taja kazi ya kujitolea ambayo umewahi kufanya na
miradi uliyofikia.
Usipopata
nafasi ya kumwona mtu unayetazamia akuajiri, acha kadi ndogo,
ikiwezekana yenye ukubwa wa sentimeta 10 kwa sentimeta 15 (business
card), ambayo ina jina, anwani, namba ya simu, na anwani ya barua-pepe,
kutia ndani maelezo mafupi kuhusu ustadi wako na mambo ambayo umetimiza.
Ikifaa, unaweza kubandika picha yako nyuma ya kadi hiyo. Wape kadi hiyo
watu ambao wanaweza kukusaidia kupata kazi na uwaombe wampe mtu yeyote
wanayemjua ambaye ana kazi unayotafuta. Mwajiri akiona kadi hiyo,
anaweza kukupa nafasi ya mahojiano, au labda akuajiri!
Kuandika
habari kuhusu elimu na ujuzi wako kunaweza kufanya uhisi ukiwa na
uhakika unapotafuta kazi. Wataalam wa masuala ya kazi wanashauri
ifuatavyo: “Kuandika habari kuhusu elimu na ujuzi wako kunaweza
kukusaidia upange mawazo na miradi yako. Pia kunafanya uwe na uhakika
kwa sababu kutakusaidia ujitayarishe kwa ajili ya maswali ambayo huenda
ukaulizwa wakati wa mahojiano ya kazi.”
Leo
hii teknolojia imerahisisha mambo. Waweza kufanya hayo yote kupitia
mtandao wa kijamii wa watu wenye taaluma ujulikanao kama LinkedIn. Mtandao huu ni maalum kwa ajili ya kukuunganisha wewe na mwajiri.
5. Jitayarishie Mahojiano Vizuri
Utajitayarishaje
kwa ajili ya mahojiano? Huenda ukataka kufanya utafiti kuhusu kampuni
unayotaka kufanyia kazi. Kadiri unavyojua mengi kuhusu kampuni hiyo,
ndivyo utakavyojieleza vizuri wakati wa mahojiano. Pia utafiti wako
utakusaidia kujua ikiwa kweli kampuni hiyo ina kazi unayotaka au kama
ungependa kuifanyia kazi.
Kisha,
fikiria mavazi utakayovaa unapoenda kwenye mahojiano. Ikiwa kazi
unayotafuta inahusisha kazi ngumu, valia mavazi safi, nadhifu, na
yanayofaa kazi hiyo. Kuvalia na kujipamba kwa njia nadhifu kutamwonyesha
mtu unayetazamia akuajiri kwamba unajiheshimu na hivyo yaelekea
utajivunia kazi yako. Ikiwa unatazamia kufanya kazi ya ofisi, vaa mavazi
ambayo huonwa kuwa yanafaa kazi hiyo mahali unapoishi. Edwini yeye
anashauri: “Chagua mavazi yako muda mrefu kabla ya wakati unapopaswa
kwenda kwenye mahojiano ya kazi ili usifanye mambo harakaharaka na kuwa
na mkazo mwingi kabla ya mahojiano.”
Pia
ninapendekeza ufike dakika 15 hivi kabla ya mahojiano. Bila shaka, si
jambo la hekima kufika mapema sana. Lakini pia kufika ukiwa umechelewa
kunaweza kuharibu mambo. Wataalamu wanasema kwamba sekunde tatu za
kwanza za mahojiano ni muhimu sana. Katika sekunde hizo, yule
anayekuhoji hukagua sura yako na tabia yako, mambo ambayo huamua maoni
yake kukuhusu. Ukichelewa, atakuwa na maoni mabaya kukuhusu. Kumbuka
kwamba hutapata nafasi nyingine ya kurekebisha maoni ambayo mtu hupata
kukuhusu mara ya kwanza.
Pia, kumbuka kwamba yule
anayekuhoji si adui yako. Huenda yeye pia alitoa ombi kwa ajili ya
kazi yake, kwa hiyo anajua jinsi unavyohisi. Kwa kweli, huenda akawa na
wasiwasi kwa kuwa labda hajazoezwa vya kutosha kuwahoji watu. Isitoshe,
ikiwa yule anayekuhoji ndiye mwajiri, huenda akapata hasara kubwa
akiajiri mtu asiyefaa.
Ili
uanze vizuri, tabasamu na umsalimu yule anayekuhoji kwa mkono ikiwa hiyo
ni desturi ya kwenu. Wakati wa mahojiano, fikiria hasa mambo ambayo
mwajiri anatarajia kutoka kwako na yale unayoweza kutimiza. Wakati wa
mahojiano, jitahidi kuyaepuka haya: Usisimame, kuketi au kutembea
kizembe. Utulivu huonyesha kwamba mtu ana uhakika. Usizungumze sana au
kwa urafiki sana, wala usitumie lugha chafu kamwe. Pia epuka kuwachambua
waajiri na wafanyakazi wenzako wa awali kwa kuwa ukifanya hivyo yule
anayekuhoji ataona kwamba utachambua kazi hiyo pia.
Wataalamu
wanapendekeza ufanye na kusema mambo yafuatayo wakati wa mahojiano:
Mtazame yule anayekuhoji, tumia ishara za kawaida unapozungumza, na
uzungumze kwa ufasaha. Jibu maswali kifupi na kwa unyoofu, na uulize
maswali yanayofaa kuhusu kampuni hiyo na kazi unayotarajia kufanya. Omba
kazi hiyo baada ya mahojiano ikiwa bado unaitaka. Kufanya hivyo
kutaonyesha kwamba bado unataka kazi hiyo.
Ukifuata mapendekezo yaliyoonyeshwa juu, huenda ukapata kazi karibuni. Ikiwa ndivyo, unaweza kufanya nini ili uidumishe?
NYONGEZA:
Jihadhari sana na kuandika mambo yasiyofaa kwenye kurasa zako katika
mitandao ya kijamii. Hii ni kwa sababu wa-ajiri wengi huwa
wanayachunguza mawazo yako kwa kuzitembelea kurasa zako katika mitandao
ya kijamii kabla na baada ya kukuita kwenye mahojiano.
Lakini
pia kama umemaliza chuo na ungependa kujiajiri mwenyewe katika biashara
pamoja na kuwasidia vijana wengine, hakikisha tunawasiliana haraka
iwezekanavyo. Wanahitajika vijana wasiozidi 3 watakaotusaidiakatika
mradi wetu wa sasa wa kukuzakiwango cha ajira hapa nchini. Kama uko Dar
es Salaam na ungependa miongoni mwa hao vijana watatu, wahi mapema.
Nipigie +255 684524265.
No comments:
Post a Comment