Ninaamini hivyo kwa sababu kuna mambo kadhaa ambayo yamenipa ushahidi kwamba, mwanaume hata akijidai kwamba ana ubavu wa kiwango gani, lakini bado kiufahamu ni mtumwa wa mwanamke. Kuna mambo makuu kama matatu ambayo yananifanya nifikiri hivyo.


Kwanza ni ile hali ya mwanaume kuweza kutawaliwa na mwanamke wa nje (aka nyumba ndogo) na kukubali kuacha familia yake na hata kuvunja heshima yake. Kuna wakati najiuliza kama kweli mwanaume mbele ya mwanamke huwa anaweza kutumia akili yoyote. Unakuta mwanaume anakutana na mwanamke barabarani na kumtongoza na akikubaliwa anamgeuza huyo mwanamke kuwa nyumba ndogo yake, lakini usidhani kwamba nyumbani kwa huyo mwanaume kuna matatizo ya ndoa. Hapana, hakuna tatizo lolote ila mwanaume huyo kaendeshwa na tamaa yake ya mwili na akashindwa kuidhibiti. Matokeo yake anajikuta analowea huko kwa nyumba ndogo yake, hadi anaharibikiwa. Hajali watoto, hajali mkewe, hajali heshima yake wala chochote.

Unakuta mwanaume anazuzuliwa na shanga tu, au kitu kingine kidogo sana, labda weupe wa mkorogo au lipstiki na makalio makubwa. Kwa ujumla utaona kabisa kwamba, ufahamu wa mwanaume ni kama ziro kabisa. Halafu kumbuka kwamba, wakati huo hiyo nyumba ndogo inajuwa kabisa kwamba, inalisanifu hilo janamume b.w.e.g.e, au tuite buzi lakini limo tu, kama GEGEREKA.

Kama mwanaume angekuwa na ufahamu kuliko mwanamke, angeweza vipi kushikwa na nyumba ndogo kwa kiwango cha kukatisha tamaa kwa kiasi hicho? Ni wazi mwanamke ndiye ambaye ana uwezo mkubwa zaidi wa kufikiri na kupanga. Kama mwanaume angekuwa na ufahamu wa kutosha, si angeweza basi kung’amua kwamba, anasanifiwa na nyumba ndogo, kwani hapo hakuna kupendwa bali kuchunwa.

Pili ni ile hali ya mwanaume kupenda kutatua mambo yake kwa mabavu badala ya kufikiri. Ukiangalia sana, kwenye matatizo au vurugu nyingi, wanawake huwa ni watu wa hekima zaidi kuliko ubabe, yaani wanatumia vichwa vyao kuliko miili. Siyo kwamba, wanaogopa kutumia miili yao, hapana. Kuna mazingira ambayo unaona kabisa kama mwanamke angeamua kujikaza hapa, hakika angempiga huyu mwanaume. Lakini sisi wanawake tunapenda kuyamaliza mambo kwa hekima na uelewano.

Hii ni hekima ambayo kwa bahati mbaya kwa wanaume wengi sana haipatikani. Kwa hiyo, unaona kabisa kwamba, mwanaume bado yuko kwenye ile hali au kiwango cha chini cha kujifahamu kwa sababu bado yuko kwenye kuamini mabavu yake.

Tatu, mwanamke ni bora zaidi kuliko mwanaume katika suala la kukabiliana na matatizo na vurugu za kimaisha. Unaweza kuona mwanamke ametelekezwa na mume akiwa na watoto, lakini hata siku moja hachukui uamuzi wa kuwakimbia watoto. Ni wanawake wachache sana kwa idadi ambayo hatuwezi kuizingatia, ambao wanaweza kufanya hivyo.

Lakini kila siku magazetini kuna taarifa za ukatili wa wanaume dhidi ya wanawake au wanaume kutelekeza familia zao. Ukiangalia sana utaona wamekimbia familia zao kwa sababu ya nyumba ndogo au kwa sababu ya ugumu wa maisha. Kwa nini msione kwamba, mwanamke bado ni shujaa zaidi ya mwanaume…?