Wafanyakazi wa migodi kugoma Afrika Kusini

Wafanyakazi wa migodi nchini Afrika Kusini
Wamiliki wa migodi ya madini nchini Afrika Kusini, wamesema kuwa wafanyakazi wao wameitisha mgomo wa kitaifa kuanzia siku ya Jumanne, kutaka mishahara yao kuongezwa................

Chama cha kitaifa cha wachimba migodi, NUM kimeitisha nyongesa ya mishahara ya hadi asilimia sitini.
Mapema wiki hii wafanyakazi hao walikataa pendekezo la waajiri wao la kutaka mishahara yao kuongezwa kwa asilimia sita, kiwango ambacho ni sawa na mfumuko wa bei kwa sasa nchini Afrika Kusini.
Afrika Kusini ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu, lakini kiwango chake kimeshuka kutokana na uwekezaji duni na uhasiano mbaya kati ya wafanyakazi na wamiliki wa migodi hiyo.
Kampuni kubwa za kuchimba madini nchini humo za AngloGold Ashanti, Gold Feilds, Harmony Gold na Sibanye na kampuni zingine ndogo ndogo tayari zimepokea ilaani hiyo ya mgomo.
Chama hicho cha NUM huakilisha asilimia sitini na nne ya wafanyakazi wa migodi wapatao elfu mia moja ishirini.
Taifa la Afrika Kusini kwa sasa linakabiliana na athari za mgomo wa wafanyakazi wa secta ya utengenezaji magari, ujenzi na wale wa viwanja vya ndege.
Wafanyakazi wa secta ya kuuza mafuta vile vile wameitisha mgomo kuanzia wiki ijayo.
Serikali ya nchi hiyo imetoa wito kwa wafanyakazi hao kudumisha amani wakati wa mgomo wao.
Mwaka uliopita, wafanyakazi thelathini na wanne wa migodi waliokuwa wakiandamana waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati ghasia zilipoibuka wakati wa mgomo wao.
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema utawala wa rais Jacob Zuma unakabiliwa na changamoto kutoka pande zote.
Wanachama wa chama chake tawala cha African National Congress ANC wanamtaka rais Zuma, kutenda zaidi ili kupunguza viwango vya umasikini, nao wafanyabiashra wanataka serikali yake kupunguza ukiritimba ili kuvutia uwekezaji kutoka mataifa ya kigeni na kuimarisha mikakati za kufufua uchumu wa taifa hilo.

No comments:

Post a Comment