Hata hivyo, saa chache kabla, baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es
Salaam waliendelea kuonja kero na adha ya kutembea kwa miguu na wengine
kulazimika kutumia fedha nyingi kupata huduma ya usafiri wa bajaj,
pikipiki, maarufu kama “bodaboda” na magari ya watu binafsi kwenda
kazini na kwenye shughuli nyingine, kuanzia saa 12 asubuhi, kabla ya
mgomo huo kusitishwa majira ya saa 7 mchana jana.
Abiria wengine walioonja kero na adha hiyo kabla ya mgomo huo
kusitishwa jana, ni wale waliotaka kusafiri kwenda katika mikoa
mbalimbali nchini, ambao kwa takriban siku mbili mfululizo walijikuta
wakisota katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) na kwenye vituo
vingine vya magari hayo vilivyoko mikoani.
Mmoja wa abiria aliyekuwa mjamzito, ambaye alitarajiwa kusafiri
kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, mkoani Kilimanjaro tangu juzi,
anadaiwa kujifungua katika kituo hicho.
Mgomo huo uliwahusu madereva wa mabasi ya masafa marefu na yanayotoa huduma maeneo ya mijini, maarufu kama daladala.
Kamati hiyo yenye wajumbe 13, iliundwa juzi na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, kuhakikisha kunakuwa na majadiliano shirikishi ya wadau
wa usafiri ili kuyapatia ufumbuzi matatizo ya barabarani.
Mengine, ambayo Makonda aliuahidi uongozi wa Uwamata, ni pamoja na
kuhakikisha majina ya wajumbe wa Umoja huo, hadidu za rejea na muda wa
mwisho wa kazi za kamati hiyo vinajulikana, kabla ya saa 4.00 asubuhi
leo, la sivyo, atakuwa mstari wa mbele kuongoza mgomo wa madereva kwa
kuwa yeye ni muumini wa migomo.
Makonda aliuhakikishia hayo uongozi wa Uwamata katika mkutano kati
yake na viongozi wa Umoja huo, uliofanyika ndani ya Kituo Kikuu cha
Mabasi Ubungo (UBT), jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk.
Makongoro Mahanga; Mkuu wa Kikosi cha Askari wa Usalama Barabarani
Tanzania, Mohamed Mpinga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura; Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare viongozi wa Uwamata; Clement
Masanja (Mwenyekiti), Shabani Mdemu (Makamu Mwenyekiti), Rashid Saleh
(Katibu), madereva, wasafiri na baadhi ya wakazi wa jijini Dar es
Salaam.
Kabla ya mkutano huo, kulifanyika kikao kati ya Makonda, Mpinga,
Kamanda Wambura na viongozi wa Uwamata nje ya ofisi ya Umoja huo iliyoko
ndani ya eneo la kituo hicho.
Kikao hicho kilifanyika ili kumpa Makonda taarifa kuhusu madai yao
na hatua walizochukua kuyafikisha serikalini na kushindwa
kushughulikiwa na serikali na hivyo kusababisha mgomo huo.
MADAI YA MADEREVA
Madai hayo ni pamoja na kupewa mikataba bora ya ajira, ambayo
itahusisha utaratibu wa ulipwaji wa mishahara ili kuisaidia serikali
kukusanya kodi tofauti na ulipwaji wa posho ambao unatumika sasa kupitia
huduma za kibenki yazinayotolewa kupitia simu za mikononi.
Wanadai utaratibu huo wa sasa umekuwa ukiwafanya wadhalilike kwa
kulipiwa na abiria chakula na kinywaji mahotelini wanapokuwa safarini.
Mengine ni kupinga uamuzi wa serikali wa kuwataka kurudi chuo kusoma wakidai kuwa hakuna jipya wanalokwenda kulisoma.
“Kama madereva kwenda shule kusoma ngazi ya digrii, diploma au cheti tutaenda kama wanavyosoma watu wengine wa kawaida.
Lakini kama ni kwenda kusoma alama za barabarani ambazo kila siku
tunacheza nazo barabarani hadi macho hayaoni kamwe hatutarudi shule,”
alisema Saleh.
Dai lingine ni kutaka mataa yaliyoko kwenye makutano ya Barabara
ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara kuachwa yafanye kazi,badala ya
magari kuongozwa na askari wa usalama wa barabarani.
Saleh alisema askari hao wamekuwa wakisababisha msongamano wa
magari katika eneo hilo kutokana na kupendelea kwa kuruhusu upande mmoja
wa magari yanayotoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) ili kuruhusu wageni na pia magari yanayotoka mjini kwenda JNIA.
kupatiwa huduma ya bima ya afya wanapopata ajali, kuingizwa kwenye
utaratibu wa kuwekewa akiba kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, kupinga
utaratibu wa kuzibana teksi pekee kulipa kodi, huku bajaj zikiachwa
kutoa huduma bila kulipa kodi.
Lingine ni utaratibu wa baadhi ya mabasi yanayotoa huduma kati ya
Dar es Salaam na nchi jirani kuishia maeneo mbalimbali yaliyoko nje ya
UBT, kama vile Kariakoo.
Dai lingine ni kupinga malori kuegeshwa kwa muda mrefu sehemu za
mipaka, kama vile Tunduma kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi, ambako alidai
wamegundua kuwa katika maeneo hayo kuna baa na nyumba za kulala wageni
zinazomilikiwa na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
hivyo kuwachelewesha kwa makusudi ili wapate kufanya biashara.
Lingine ni ukaguzi wa magari kufanyika mara moja kwa wiki ili
kuondoa adha za magari kukamatwa mara tatu kwa siku na kuandikiwa malipo
ya faini za mara kwa mara, ambao wanadai wakati mwingine ukaguzi huo
umekuwa ukifanywa kwa makusudi, hasa katika maeneo ya bandarini.
"Tulitaka waziri mkuu aje atatue mgogoro huu, lakini kumbe kuna
ambaye anaweza kuutafutia ufumbuzi, lakini cha msingi sisi si kumtafuta
waziri mkuu bali kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili, ikizingatiwa kuwa
ugomvi wetu siyo sisi na serikali, bali na wamiliki ambao wanatakiwa
kutupatia haki zetu za msingi," alisema Saleh.
VURUGU ZAZUKA, MMOJA ANG’ATWA NA MBWA WA POLISI
Hata hivyo, wakati uongozi wa Uwamata wakiendelea kumpa maelezo
Makonda, askari polisi wa kikosi cha mbwa walifika na kuanza kuwatawanya
madereva waliokuwa wamesimama pembezoni mwa eneo ambalo kikao hicho
kilikuwa kikiendelea.
Kitendo hicho kilizua tafrani kubwa baada ya madereva hao kupinga
kufukuzwa eneo hilo na kuanza kuwarushia askari hao mawe mfululizo.
Askari hao walijibu mashambulizi kwa kufyatua risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi.
Katika vurugu hizo, watu wawili waling’atwa na mbwa wa polisi;
mmoja sehemu ya kiuno, mwingine kidole na mwingine kujeruhiwa na jiwe
kichwani.
No comments:
Post a Comment